Fikra za Mustakabali wa Kiafrika
Ni zaidi ya simulizi-bunifu ya kisayansi kutoka kwa mtu mweusi

Fikra za Mustakabali wa Kiafrika katika filamu: Kipande cha picha kutoka kwenye filamu ya Marvel ya Black Panther
Fikra za Mustakabali wa Kiafrika katika filamu: Kipande cha picha kutoka kwenye filamu ya Marvel ya Black Panther | Picha (maelezo): © picture alliance/AP Photo

Dunia za kesho mara nyingi huonekana kuumbwa kwa dira za Magharibi za majaaliwa ya mwanadamu. Fikra za Mustakabali wa Kiafrika hutoa mbadala ambao unasisitiza jinsi gani tanzu iliyozoeleka ya simulizi-bunifu ya kisayansi ilivyoimarishwa na ilivyo vigumu kuibadilisha. Dira hii yenye mvuto wa Kiafrika inajenga msingi katika filamu, riwaya na muziki, na ina maana kubwa sana zaidizaidi ya kuwapeleka tu katika anga za mbali wahusika wakuu Weusi.
 

Istilahi ya simulizi-bunifu ya kisayansi kwa kawaida unahusianishwa kimiujiza na ndoto za siku zijazo zenye vyombo vya anga vikipishana katikati ya za ulimwengu, awajenzi wa kesho wakitengeneza mmakazi mapya kwa ajili ya wanadamu, na maroboti yakiwa sehemu kamili za maisha ya kila siku.  Taswira hizi kwa ujumla wake zinaumbwa kutokana na dhana na fikra za  Magharibi, ambapomustakabali mzima unahusiana na maendeleo, uvumbuzi wa kiufundi na kuanzisha ukoloni kwenye sayari mpya, na kwa nadra sana kuhusiana na uboreshaji wa hali za maisha za makundi yanayofanyiwa udhalimu. Fikra za Mustakabali wa Kiafrika zinaonesha jinsi dira yetu tofauti ya dunia ya kesho inavyoweza kuwa.

Mtu mweusi katika mustakabali

Katika filamu, riwaya, mitindo, muziki, sanaa za uchoraji, uchongaji na ufinyanzi na maonesho ya jukwaani, Fikra za Mustakabali wa Kiafrika zinasawiri jamii ambazo watu Weusi wanaweza kuishi kwa usawa. Mkosoaji wa utamaduni wa Kimarekani aitwaye   Mark Dery aliunda istilahi hii mnamo mwaka 1994 katika insha yake ya Mtu Mweusi katika Mustakabali, ambapo alionesha Wamarekani wenye asili ya Kiafrika kama wataalamu katika fani ya simulizi-bunifu ya kisayansi, na kuuliza kwa nini kulikuwa na watunzi wachache sana wa simulizi-bunifu ya kisayansi miongoni mwa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika. Katika maelezo yaliyonukuliwa kwa mapana kuhusiana na Fikra za Mustakabali wa Kiafrika, mwanamuziki na mwandishi Greg Tate alirejelea maisha kama mtu Mweusi nchini Marekani katika mahojiano kwa kusema: “Kitendo cha kuwa Mtu Mweusi nchini Marekani chenyewe peke yake ni uzoefu wasimulizi-bunifu ya kisayansi.”
 
Wasanii wengi Weusi wanaelezea dhima yao kufanana sawa na ile ya “kiumbe wa ajabu kutoka dunia nyingine” katika   jamii ya Magharibi. Mfanano huu unadhihirika hasa nchini Marekani, ambapo neno lenye maana ya “kiumbe wa ajabu kutoka dunia nyingine” ni neno rasmi linalotumiwa na serikali ya Marekani likiwa na maana ya watu kutoka nchi nyingine, na pia likimaanisha viumbe kutoka anga za mbali. Dhana ya kujihisi kuwa kiumbe wa ajabu kutoka dunia nyingine ukiwa katika nchi yako mwenyewe ina mzizi wake katika historia ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, kwa wahenga wao kutekwa kutoka Afrika na kuletwa Marekani kama watumwa ambapo hawajawahi kamwe kutendewa kwa usawa. Mtunzi na mwandishi wa habari wa a Kiingereza aitwaye Kodwo Eshun anatoa mfanano sambamba unaoonekana kwa uwazi zaidi: “Kama vile roboti (...), kiuhalisia mtumwa alitengenezwa ili kutekeleza kazi: kama mtambo, kama mfumo wa usafiri (...). Watumwa ni viumbe wa ajabu kutoka dunia nyingine.”

Mwanazuoni wa fasihi ya Kijerumani anayeitwa Peggy Piesche anadokeza kwamba Fikra za Mustakabali wa Kiafrika mara nyingi hutafsiriwa visivyo kama simulizi-bunifu ya kisayansi ya Mtu Mweusi ambapo waigizaji Weusi hupangiwa uhusika katika dhima za kimapokeo. Lakini Fikra za Mustakabali wa Kiafrika zinapaswa kueleweka zaidi kama harakati pinzani inayovumbua dunia mpya kabisa za simulizi-bunifu ya kisayansi.

Fikra za Mustakabali wa Kiafrika kutoka majumba ya  maonesho ya Ujerumani

Tangu miaka 1990, wasanii na wabunifu wengine wamejihusisha na ya simulizi-bunifu ya kisayansi ya Kiafrika. Suala hili limeangaziwa katika mihadhara makini juu ya  utamaduni wa sanaa pendwa, ubaguzi wa rangi, utetezi wa nadharia ya haki na usawa wa wanawake, na katika jamii, zaidi nchini Marekani na Kanada, na kutoka nchi nyingine zinazotumia Kiingereza, na liliongelewa katika kongamano la Loving the Alien  liliondaliwa na Diedrich Diedrichsen katika Jumba la Maonesho la Volksbühne mjini Berlin mwaka 1997. 

Tokea wakati huo, majumba ya maonesho ya Ujerumani yameonesha mahsusi michezo ya kuigiza yenye mada zinazohusu Mustakabali wa Kiafrika, ambapo wasanii vijana kama mtunzi Olivia Wenzel huongelea jinsi masimulizi mbadala yanavyoweza kutumia anga za mbali kama tamathali za kufikiwa kwa jamii timilifu ya kufikirika yenye usawa. Katika picha yake ya maonesho iliyotengenezwa kwa kugandishwa vipande vipande anayoiita Sisi ni Ulimwengu, ambayo inatokana na maandishi, filamu mbalimbali na nadharia za simulizi-bunifu ya kisayansi ya Mtu Mweusi, anagusia matukio ya hivi karibuni kama vile Safari ya Mars.

katika mchezo wa kuigiza unaotetea nadharia ya haki na usawa wa wanawake ambao unaitwa Mwanamke Mweusi wa Kwanza Anga za Mbali, mwigizaji wa Kijerumani anayeitwa Simone Dede Ayivi anataza nyuma katika historia ya Afrika na a wanadiaspora wa Kiafrika ambapo pia anaongelea hali ya  wanawake Weusi wa  siku za leo. Katika simulizi za vuguvugu la mabadiliko na uwezeshaji, Ayivi na kundi lake wanaonesha kwamba wanawake Weusi wa kuigwa mfano siyo wachache, bali wanapitia tu uwakilishi wa chini kuliko kiwango katika utambuzi wa umma.

Kipande cha picha kutoka kwenye mchezo wa kuigiza “Sisi ni Ulimwengu” uliooneshwa katika Jumba la Maonesho la mjiniBallhaus Naunynstraße mjini Berlin Kipande cha picha kutoka kwenye mchezo wa kuigiza “Sisi ni Ulimwengu” uliooneshwa katika Jumba la Maonesho la mjiniBallhaus Naunynstraße mjini Berlin | Picha (maelezo): © Zé de Paiva Siyo filamu ya STAR WARS ya mtu mweusi

Fikra za Mustakabali wa Kiafrika katika lugha zote mbili za Kijerumani na Kiingereza hutofautina kimsingi na simulizi-bunifu ya kisayansi ya Magharibi. Hazitilii chumvi kabisa desturi, visa-asili na hata sanaa za jadi kwa kuepuka sifa za kiroboti na rangi za kumetameta. Badala yake kuhifadhi sifa za Kiafrika kama vile mavazi ya kitaifa, usanifu wa majengo na madhari ni tabia mojawapo ya Fikra za Mustakabali wa Kiafrika.  

Filamu kama vile Star Wars zinajenga taswira kamili ya dunia za kufikirika, lakini simulizi-bunifu ya kisayansi ya Mustakabali wa Kiafrika imeota mzizi imara utokanao na hali halisi. Kama aina ya sanaa, inasawiri dunia ambayo ndani mwake watu wenye asili ya Kiafrika wanaasi dhidi ya mustakabali kamili wa Kizungu na kupigania usawa. Mwandishi na mtunzi wa kitabu Afrofuturism: The World of Black Sci-Fi & Fantasy Culture, Ytasha Womack, anaeleza kwamba Wafuasi wa Mustakabali wa Kiafrika kimsingi wamejikika katika kubadili hali za kijamii, tofauti za kitaifa na rangi. Anachukulia “uwezeshaji” kama msingi wa kujiongoza. Wasanii kama Ingrid LaFleur na Martine Syms hawaoni mustakabali katika anga za mbali. Kupitia filamu yake ya Mundane Afrofuturist Manifesto, Syms aliumba aina fulani ya mbadala wa kidunia katikati ya anga la nyota, mbadala mojawapo inayoleta majaaliwa ya Mustakabali wa Kiafrika katika upeo unaofikika na siyo dunia ya kufikirika iliyopo umbali unaokaribia maili milioni 6.