Mazingira ya kazi katika sanaa
Haki katika biashara ya muziki wa kupakua mtandaoni

Katika hali ya kawaida, mazingira ya kazi kwa wasanii mjini Berlin ni magumu, na wachache tu miongoni mwao ndio wanaoweza kuendesha maisha yao kupitia kazi zao za sanaa peke yake.
Katika hali ya kawaida, mazingira ya kazi kwa wasanii mjini Berlin ni magumu, na wachache tu miongoni mwao ndio wanaoweza kuendesha maisha yao kupitia kazi zao za sanaa peke yake. | Picha (maelezo): © picture alliance/Paul Zinken/dpa

Wasanii wengi wanaishi katika mazingira ya mashaka, na wachache tu miongoni mwao ndio wanaoweza kuendesha maisha yao kupitia kazi zao za sanaa. Harakati kama vile za watoaji wa muziki kwa haki na hati za haki katika biashara kwa makampuni ya muziki zinaonesha jinsi mnyororo wa thamani wenye usawa zaidi unavyoweza kutengenezwa.

Wakati ambapo leo hii kuna mamilionea zaidi wa YouTube na wasanii vijana wenye shauku ya kung’aara kuliko ilivyowahi kutokea awali, wengi miongoni mwa wasanii nchini Ujerumani wanaishi maisha ya mashaka. Wengi wanalalamika kwamba urasimu unawawekea viunzi, shinikizo katika masoko yenyewe, na ushindani unaongezeka kila kukicha. Jambo hili linajitokeza wazi hasa mjini Berlin, jiji lenye asilimia kubwa isiyo ya kawaida ya wasanii, hata kwa viwango vya kimataifa. Kwa miaka kadhaa, gharama za chini za kukodi studio ziliwashawishi wasanii kuhamia kwa wingi katika jiji hilo, lakini sasa gharama zinapanda. Ingawa nafasi kwa ajili ya makazi ya kuishi mjini Berlin bado inapatikana kwa gharama za chini zaidi ikilinganishwa na London au Paris, wastani wa kodi umepanda karibia mara mbili ya hapo awali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kutoka yuro 5.20 hadi yuro 9.50 kwa mita moja ya mraba. Berlin inashika namba moja nchini Ujerumani, ukiongoza nchini katika kasi kubwa ya ongezeko la kodi, japo majiji kama Hamburg na Frankfurt nayo pia ilirekodi ongezeko la kasi la kodi linalofikia asilimia 50.
 
Mwaka 2018, Taasisi ya Berlin ya Maendeleo ya Kimkakati ilichapisha taarifa ya utafiti juu ya mazingira ya kazi katika fani ya sanaa ya uchoraji: “ Mazingira ya Wasanii wa Berlin na Pengo la Jinsia”. Iligundua kwamba asilimia 80 ya wale wanaofanya kazi katika sekta ya sanaa ya uchoraji mjini Berlin hupoteza fedha katika kazi zao za sanaa, na mmoja tu kati ya kumi ndiye aliyeripotiwa kuwa na uwezo wa kuendesha maisha kwa mwaka mzima kupitia kazi zao za sanaa. Kwa wastani, wanawake wanaingiza kipato ambacho ni pungufu kwa theluthi moja kuliko wanaume. Kwa kuongezea, utafiti huo unatabiri kwamba takribani asilimia 90 ya zaidi ya wasanii1,700 waliotoa maoni yao, hatimaye wataangukia katika lindi la umaskini nyakati za uzeeni ambapo wastani unaotarajiwa wa kiinua mgongo ukiwa ni yuro 357 tu kwa mwezi.

Dhana iliyozoeleka ya ‘msanii mwenye njaa’ siyo tu inatokana na uhalisia, bali inaonekana pia kuwa kanuni badala ya kuwa kikwazo. Pengine kama matokeo yake, ndiyo maana vuguvugu la kampeni ya biashara ya haki katika sanaa linaongezeka – kwa mfano katika biashara ya muziki.

Uchaguzi wa mteja unaweza kuzaa tofauti

Wadau wengi wanahusika kwenye mnyororo wa thamani wa muziki wa kupakua mtandaoni, ikijumuisha makampuni ya muziki, wasambazaji, majukwaa, vyama vya hakimiliki, mawakala na mameneja. Katika soko linalokanganya la huduma ya upakuaji na matangazo ya sauti kwa njia ya intaneti, ukubwa wa kipande cha mkate kinachomfikia msanii hutofautiana sana.  
 
iTunes, kwa mfano, hulipa  kiasi kinachofikia theluthi mbili ya mapato ya kampuni hiyo yanayotokana na mauzo kwa mwandishi wa wimbo, lakini hutoza ada kubwa mno ya mwaka kama malipo ya huduma, ambayo ni ngumu hasa kwa makundi madogo zaidi kulipa. Jukwaa la taarifa kwa njia ya picha “Information is Beautiful”  linakadiria kwamba ni sharti kwa nyimbo za msanii wa kujitegemea kupakuliwa hadi mara 1,826 kwa mwezi kutoka iTunes ndipo aweze kujiingizia kipato kinacholingana tu na kima cha chini cha mshahara unaolipwa nchini Marekani. Miongoni mwa watoaji wakubwa wa huduma, jukwaa mubashara la Bandcamp hutoa mgao mkubwa kuliko wote wa mapato, asilimia 85, kwa wanamuziki.
 
Majukwaa ya muziki yanayojipambanua katika mazingira ya haki hutoa an mbadala. Mfano ni lile la igroove, linalochipukia nchini Uswisi, ambalo hutoa fursa kwa nyimbo za wanamuziki zaidi ya 3,000 kupakuliwa na wasikilizaji katika mazingira ya haki. Asilimia 92 kamili ya mapato huenda moja kwa moja kwa wasanii, na wapenzi wa muziki wanaweza pia kuwaunga mkono wasanii wao wanaowavutia zaidi kwa kulipa fedha zaidi endapo wanapenda. Ushirika wa Resonate ni uchaguzi mwingine. Badala ya mtindo wa kulipia kwa mwezi, wao walitengeneza mfumo wa kipekee wa ‘sikiliza ili umiliki’. Wasikilizaji hulipia kiasi kidogo kila wakati wanaposikiliza wimbo. Baada ya kusikiliza mara tisa, wimbo unakuwa umelipiwa kikamilifu na unaweza kupakuliwa kutoka kwenye jukwaa. Katika jukwaa la Resonate, wanachama wote – wasanii, makampuni na wapenzi wa muziki – hupanga kanuni kwa pamoja na kugawana faida miongoni mwast mwao wenyewe.

Busker in Berlin. Busker in Berlin. | Picha: © picture alliance/imageBROKER Hatimaye, nguvu inatokana na wateja. Lakini mara nyingi wanakosa taarifa wanazohitaji ili waweze kufanya uchaguzi wa kimaadili. Kwa hiyo, Shirika la Kanada la Biashara ya Haki katika Muziki Kimataifa (FTMI) limetengeneza hati ya biashara ya haki katika muziki. Kama inavyofanyika katika desturi ya haki kwenye biashara ya bidhaa kama chakula, kunakuwa na nembo inayotoa hakikisho kwamba kampuni husika ya muziki hugawa faida kwa haki kwenda kwa wasanii. Walau asilimia 80 ya mapato ni sharti ilipwe kwa ajili ya haki ya kutumia muziki ili kupata muhuri huo.
 
Shirika la FTMI sasa linaungwa mkono na wanamuziki nusu milioni kutoka duniani kote, lakini kampuni moja tu ya muziki ndiyo imepata imepata hati. Wachapishaji wengi wa muziki wanaona mchakato wa kupata cheti kuwa mgumu sana, linasema shirika hilo. Miongoni mwa mambo mengine, ni vigumu kuyashawishi makampuni makubwa ya muziki na huduma za matangazo ya sauti kupitia intaneti kuweka wazi taarifa zao za kifedha kama mchakato wa kupata hati unavyohitaji.

Kuzingatia kwa hiyari haki za kimsingi za kazi

Chama kinachojiita “Sanaa lakini Haki” kinajaribu kuchukua mkondo tofauti nchini Ujerumani, Austria na Uswisi, na kinajikita awali na kwa umuhimu katika kuinua uelewa. Kupitia harakati kama vile “Künstler-Klagemauer” (mahali ambapo wasanii wanaweza kupata faraja), ukurasa wa Facebook ambapo wasanii wanaweza kutuma chochote kuhusiana na uzoefu wao wa mazingira ya kazi yasiyo ya haki, au tuzo za “Goldene Stechpalme” zinazotolewa kwa matukio ya kutia huzuni na kushtua kuliko yote katika muziki na sanaa za kuonesha jukwaani, chama hiki kinataka kuelekeza jicho la siasa na jamii kwenye manung’uniko. Lengo la chama hiki ni kubuni hati itakayotolewa kwa taasisi za utamaduni zenye mazingira ya kazi yanayotoa haki kwa matumaini kwamba ufadhili wa serikali wa shughuli za utamaduni utazingatia muhuri huu wa ubora katika siku za baadaye.

Hadi kufikia hapo, uchaguzi pekee kwa wasanii ni mkataba wa hiyari ambao chama kimeuandaa, wenye kifungu kinachowataka watia saini kuwa na kawaida ya kuwasilisha katika ofisi za chama ripoti za maendeleo. Kama malipo ya huduma, majina yao yamechapishwa kwenye tovuti. Washirika wa mkataba wanaafiki kukubali mahusiano ya ajira yanayozingatia tu mshahara sahihi na kuhimiza juu ya utii wa sheria za kazi. Mkataba umekusudiwa siyo kwa wasanii tu, bali pia kwa waajiri na wanasiasa wanaojihusisha na kitamaduni. Mameneja, wakurugenzi na mwanasiasa mmoja tayari wamesaini makubaliano kwa upande wao binafsi.