Kutengeneza maudhui ya kidijitali katika Sanaa
“Ugumu wa mambo ndiyo uzuri wake”

Vipi endapo maisha ya Fred yamekuwa tofauti? Katika onesho la uzinduzi la Kay Voges la Die Parallelwelt, watazamaji waliona hadithi mbili za maisha kwa wakati mmoja – moja ikioneshwa mubashara jukwaani, nyingine ikiwasilishwa kupitia kioo cha videokioo cha video.
Vipi endapo maisha ya Fred yamekuwa tofauti? Katika onesho la uzinduzi la Kay Voges la Die Parallelwelt, watazamaji waliona hadithi mbili za maisha kwa wakati mmoja – moja ikioneshwa mubashara jukwaani, nyingine ikiwasilishwa kupitia kioo cha videokioo cha video. | Picha (maelezo): „Die Parallelwelt“, Kay Voges © Birgit Hupfeld / Schauspiel Dortmund

Uhalisia wa kutengeneza, picha za 3D na teknolojia ya roboti vimekuwa vikitumiwa kwa muda mrefu na waongozaji wa sanaa za maonesho katika nchi nyingine lakini  bado havijachangamkiwa kama nyenzo au mbinu za uzalishaji wa kazi za jukwaani nchini Ujerumani. Jambo hili linakaribia kubadilika. Kituo kipya cha Akademie für Digitalität und Theater (Kituo cha Utengenezaji wa Maudhui ya Kidijitali na Sanaa za Maonesho) katika jiji la Dortmund kimejipanga kufanya mapinduzi katika duru ya sanaa za maonesho nchini Ujerumani. 

Vipi endapo maisha ya Fred yamechukua mkondo tofauti? Katika onesho la Die Parallelwelt (“Dunia Mbili Sambamba”), uliooneshwa kwa mara ya kwanza mwezi Septemba 2018, swali hilo linachunguzwa na makampuni mawili ya sanaa za maonesho kwa pamoja – katika majiji ya Berlin na Dortmund. Yote mawili yanasimulia hadithi ya maisha ya Fred lakini zinawaslisha matoleo tofauti: mkondo wa maisha yake unaongozwa na bahati tu. Majumba mawili ya maonesho yanaunganishwa kwa kilometa 420 za mkongo wa mawasiliano, unawezesha kile kinachotokea katika jukwaa moja kurushwa mubashara katika jumba jingine la maonesho. Watazamaji hufuatilia hadithi zote mbili kwa wakati mmoja – moja ikioneshwa jukwaani, nyingine ikioneshwa  katika kioo cha video. 
 
Jumba la maonesho ni njia ya analojia ya mawasiliano lakini kama onesho la Kay Voges la Die Parallelwelt linavyoonesha, inaweza kusukwa katika uhalisia wa kutengeneza. Mbinu za kidijitali za kuongoza uzalishaji wa kazi za jukwaani pamoja na majaribio vimemfanya awe mwasisi nchini Ujerumani – na anaufahamu vizuri ukweli huo: “Kwa viwango vya kimataifa, duru ya sanaa za maonesho nchini Ujerumani ina mambo mengi ya kuangalia linapokuja suala la uvumbuzi wa kidijitali. Katika nchi nyingi, matumizi ya kompyuta katika kutatua changamoto yana mchango mkubwa zaidi kwenye kazi za sanaa za maonesho kuliko mahali hapa.”
 

Tangu Voges alipokuwa mkurugenzi wa stadi za ubunifu wa Schauspiel Dortmund, timu ya wataalamu wa fani tofauti katika taasisi hiyo imekuwa ikifuatilia fursa zinazopatikana kutokana na mapinduzi ya kidijitali. Voges anaamini hilo ni jambo la kutazamwa kwa haraka endapo tunataka sanaa za maonesho kuendelea kuwa  kuwa na maana: “Nafikiri ni haki kusema kwamba mageuzi katika jamii kufuatia mwamko wa kutengeneza maudhui ya kidijitali ni makubwa kama mabadiliko yaliyoletwa  na uvumbuzi wa viwanda vya uchapaji. Ni jinsi gani sanaa ya maonesho inaweza kugusa matatizo na migogoro ya jamii ya sasa endapo sanaa hiyo haiwezi kwenda na kasi ya hayo maendeleo ya jamii? Sasa inahitajika zaidi ya mbinu za masimulizi za kabla ya nyakati za kidijitali ili kuonesha ugumu wa mambo katika maisha.”

Mafunzo ya utengenezaji wa maudhui ya kidijitali kwa ajili ya sanaa za maonesho 

Lakini Voges anajua kutokana na uzoefu wa muda mrefu ni matatizo gani ambayo majumba ya maonesho hukabiliana nayo linapokuja suala la kutengeneza maudhui ya kidijitali. Kwa mzunguko wa kawaida wa mazoezi yanayochukua wiki sita hadi nane, ni vigumu kupata muda wa kutosha au fedha kwa ajili ya majaribio halisi. Kuna pia uhaba wa wataalamu wenye ujuzi katika maeneo yote, kuanzia uhalisia wa kutengeneza na kurekodi miondoko hadi teknolojia ya roboti na uwezo wa kiakili wa kompyuta - ambalo siyo jambo la kushangaza ikizingatiwa kumekuwa hakuna programu za mafunzo ya stadi za kidijitali kwa zaidi ya watu 40,000 wanaofanya kazi katika majumba ya sanaa za maonesho nchini Ujerumani. “Injinia wa mwanga aliyeajiriwa kama fundi umeme miaka 25 iliyopita sasa anakaa katika jopo linaloshughulika na programu ya mwanga unaohamishika. Na injinia wa sauti ambaye alizoea kusikiliza kaseti ya sauti wakati wa maonesho sasa naye pia anafanya kazi kwa kutumia kompyuta.”
 
Kuziba pengo lililopo kati ya utaratibu wa kawaida wa majumba ya sanaa za maonesho na fursa zinazopatikana kupitia teknolojia za kidijitali, Voges na timu yake – baada ya awamu ya kwanza ya miaka mitatu –  wameanzisha kituo cha Akademie für Digitalität und Theater mjini Dortmund. Mwezi Machi 2019, kitaendesha programu za mafunzo kwa mafundi mitambo wa sanaa za maonesho na wasanii kwa kushirikiana na chama cha wataalamu wa ufundi mitambo kwenye sanaa za maonesho cha Kijerumani  DTHG na chama cha waajiri katika sanaa za kuonesha jukwaani Deutscher Bühnenverein. Kwa kuongezea katika muhtasari mkuu wa kozi, Septemba 2019 itashuhudia wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma kwa ufadhili wakiingia katika miradi ya majaribio ya utafiti katika stadi za ubunifu. Ipo siku, kituo kitaendesha pia programu ya shahada ya sanaa katika habari kupitia maonesho – lakini Voges anakiri kulifikia jambo hilo “bado kuna safari ndefu”.
 
Hadi majengo mapya yanayojengwa katika mji wa bandari wa Dortmund yatakapokamilika mwaka 2020, kituo kitaendelea kutumia majengo ya muda yaliyotolewa na Schauspiel Dortmund. Kigezo kwamba mji Dortmund, ukiacha miji mingine yote, umejipambanua wenyewe kama kitovu cha cha sanaa za maonesho na utengenezaji wa maudhui ya kidijitali kinatokana na historia ya jiji lenyewe: eneo la makao makuu ya Ruhr linakumbuka miaka 700 iliyopita ya uchimbaji wa madini, iliyofikia   tamati kufuatia kufungwa kwa mgodi wa mwisho wa makaa ya mawe mwaka 2018. Mji wa Dortmund ulitarajia mabadiliko makubwa sana mbele yake na ulichukua hatua za awali za kulinda mustakabali wake, ukawa kituo cha kidijitali cha tano kwa ukubwa kuliko vyote nchini Ujerumani. 

Fursa siyo kitisho

Ubashiri wa fursa zisizo na mwisho zinazotengenezwa pale teknolojia ya kidijitali na sanaa za maonesho vinapoletwa pamoja ulitolewa katika kongamano lililoitwa Enjoy Complexity lililoandaliwa kwa pamoja baina ya Voges na Schauspiel Dortmund katika maadhimisho ya kufunguliwa kwa kituo hicho wakati wa majira ya kuchipua ya mwaka 2018. Miongoni mwa mambo mengine, wageni walitambulishwa moja kati ya kazi za Voges za uhalisia wa kutengeneza. Wasanifu wa njia za mawasiliano walikuwa wametengeneza skana za jukwaani zilizowekwa kwa ajili ya onesho la Die Borderline Prozession, ambazo zilichukua video za matukio kutoka nyuzi 360° walizoziunganisha na kuzifanya kuwa kazi ya uhalisia wa kutengeneza ya sanaa za maonesho. Kwa kutumia miwani ya kuangalizia uhalisia wa kutengeneza, mtazamaji anaingizwa mara moja katika matukio ya onesho, akiwa na uwezo wa kutembea kwa uhuru jukwaani na ukumbini wakati mchezo ukichukua mkondo wake. 
 
Hata hivyo, kituo cha Akademie für Digitalität und Theater hakitajikita tu katika fursa zinazoletwa na teknolojia. Voges anaiona dhima yake pia kuwa kama ya kisiasa – kuchunguza masuala kama vile kubadilisha picha kwa hila, faragha na mitandao ya kijamii. “Ninapoangalia mazingira ya kisiasa nchini Ujerumani na Ulaya ninaona mwenendo wa kupunguza makali”, anaelezea. “Masuala yanarahisishwa, kuoneshwa kwa urahisi kuliko jinsi yalivyo kwa hakika. Nachukulia siasa za kutaka kumfurahisha kila mtu kama mwitikio hatari wa hofu ya utandawazi na dhidi ya kutengeneza maudhui ya kidijitali kwa jamii. Sanaa za maonesho ni mahali ambapo ugumu wa mambo unaweza kuonekana kama fursa, siyo kitisho. Ugumu wa mambo ndiyo uzuri wake.”