Miaka 250 ya Alexander Von Humboldt
Nyufa kwenye Makumbusho

Sauti za uchambuzi zinameguka kutoka kwenye sanamu ya mwanasayansi Alexander von Humboldt.
Picha (maelezo): © picture-alliance/dpa-Zentralbild/Heinz Krimmer

Alexander von Humboldt anapendwa na watu wengi wenye shauku, lakini wapo pia wakosoaji. Kwenye maadhimisho ya miaka 250 tangu kuzaliwa kwa nyota huyu wa sayansi, wataalam wanaonya kuwa umashuhuri wake kama binadamu umetiwa chumvi, japo hakuna anayepinga mafanikio yake kama mtafiti.

Kutoka juu ya maghorofa katika mji wa Ciudad Bolivar ambao ni kitovu cha utalii nchini Venezuela, wageni wanaweza kujionea delta ya Mto Orinoco na msitu ulioshamiri nyuma yake. Wakati wa msimu wa mvua, hali ya unyevu hukaribia asilimia 100 na joto huwa chini kidogo ya nyuzi 30, hata nyakati za usiku. Siyo vigumu kujenga picha ya majaribu na taabu alizopitia Alexander von Humboldt mnamo Februari 1800 katika safari yake ya ugunduzi ya kuvuka mto Orinoco akitokea Caracas kuelekea Rio Negro. Ilikuwa safari ya kwanza ya ugunduzi kufanywa na mwanasayansi wa Berlin, iliyochukuliwa na wengi kuwa ni ugunduzi wa kisayansi wa Amerika Kusini, na ulikuwa mwanzo wa kazi ambayo hatimaye iliishia kumpatia umaarufu ulimwenguni kote.

Shauku ya dhati juu ya mgunduzi huyu ambaye pengine ndiye mtu wa kwanza mashuhuri kutoa mchango wa kitaalamu kwenye historia ya sayansi na mmoja miongoni mwa wasomi wanaotambulika ulimwenguni inaendelea kushamiri hata sasa. Mambo aliyoandika juu ya mwingiliano unaokubaliana kwa asili, kumbukumbu za safari zake na shauku ya kufanya mambo ya ujasiri vimepelekea kuacha simulizi nyuma yake. Vyuo vikuu na shule mbalimbali, na hata sehemu mojawapo juu ya uso wa mwezi, vimepewa majina kwa heshima yake. Siku ya tarehe 14 Septemba 2019, jumla ya mishumaa 250 ingeweza kupamba keki ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa kupuliza kwa mdomo ili kuizima mishumaa yote hiyo pengine ingechukua muda kiasi, taasisi inayoitwa kwa jina lake iliutangaza mwaka 2019 kuwa mwaka wa Humboldt. Matukio mengi katika kipindi cha mwaka mzima yatatumika kuenzi kazi za mwanasayansi huyu ambaye ni mtoto wa askari mashuhuri aliyehudumu kwenye jeshi la Ufalme wa Prussia.

Picha: © picture alliance/akg-images Samaki aina ya mkunga wakichupa kuwakabili farasi ndani ya Mto Orinoco. Kwa jaribio hili, von Humboldt alithibitisha kwamba mkunga hushambulia pia wanyama wa nchi kavu. Mchoro wa kwenye ubao tangu 1870.

Andrea Wulf anaeleza kinagaubaga maono ya uvumbuzi ya mtafiti huyu katika kitabu chake maarufu kiitwacho ‘The Invention of Nature: Alexander von Humboldt’s New World, and the second volume, The Adventures of Alexander von Humboldt’. Kwa mfano, anadai kwamba Humboldt alitabiri "mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababishwa na binadamu tangu mwaka 1800." Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mwaka wa kumbukizi ya Humboldt nchini Ecuador, Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier alisema: "Alikuwa mmoja wa wataalamu ambao dunia imepata kuwafahamu, mwenye uwezo wa kuifafanua asili."

“Humboldt anakuzwa mno”

Baadhi ya wanasayansi wanaona kwamba sifa ya Humboldt imejazwa upepo. Matthias Glaubrecht, mkuu wa Kituo cha Historia ya Asili katika Chuo Kikuu cha Hamburg anasema, "Bila la kuvunja heshima - Humboldt amekuzwa mno." Wakati ambapo mwandishi Wulf anamwona Humboldt kama mtu “aliyevumbua asili” na aliyetabiri athari za mabadiliko ya tabianchi zitokanazo na binadamu, mwanazuolojia Glaubrecht anabisha, "Humboldt alikuwa na uelewa tofauti kabisa wa dunia. Alipingana na wazo la maendeleo.” Anaongezea kuwa, kulikuwa na sababu ya msingi kwa nadharia ya Darwin ya mwaka 1859 ambayo ndiyo ya karibuni zaidi kuchukua nafasi badala ya ufafanuzi wa Humboldt kuhusu asili, katika mwaka ambao Humboldt alifariki. Hata maono ya Humboldt kutoka kwenye safari zake za ugunduzi huko Venezuela kuwa ufyekaji wa misitu ana athari katika hali ya hewa hayawezi kupoleweka vema kama onyo juu la kasi inayoongezeka ya mabadiliko ya tabianchi, Glaubrecht anasisitiza.

Kibaraka wa Ukoloni?

Picha ya mwanasayansi Alexander von Humboldt iliyochorwa na Friedrich Georgia Weitsch, 1806 Picha ya mwanasayansi Alexander von Humboldt iliyochorwa na Friedrich Georgia Weitsch, 1806 | Picha: © Wikipedia, gemeinfrei Mtazamo wa Humboldt kuhusu utumwa na ukoloni pia ni una utata. Kwa mfano, vuguvugu la “No Humboldt21” linapingana na mpango uliopo wa uzinduzi wa jengo la Humboldt Forum huko Berlin, sababu mojawapo ikiwa ni kuhoji uhalali wa jina la jengo hilo. Makumbushusho hiyo mpya na kubwa kuliko zote nchini Ujerumani iliyopo kwenye kasri la Berlin lililojengwa upya inatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwaka 2019 na itakusanya vitu vyote vya ukumbusho katika jiji hilo vilivyokusanywa nje ya Ulaya. Moja ya maazimio ya vuguvugu la “No Humboldt21” linatamka kuwa ugunduzi wa maeneo fulani duniani uliofanywa na watafiti wa Kizungu ulichangia kwa kiasi kikubwa unyonyaji wa maeneo hayo: “Kulingana na mtindo ulioonekana kufaa kwa wakati huo, ‘wagunduzi halisi wa Amerika’ kutoka Prussia waliokwenda mbali zaidi kiasi cha kufukua miili na kuisafirisha hadi Ulaya, wanaupamba utawala wa kikoloni.” Zaidi ya hayo, wanaharakati wanadai kuwa Mfalme wa Hispania iliunga mkono safari za utafiti za Humboldt. Ili aweze kupata vibali vya kufanya safari kwa ukamilifu, Humboldt aliacha kufanya ukosoaji wake wa kisiasa. Wanaharakati wanadai kuwa Mfalme wa Hispania alinufaika pia kutokana na taarifa alizotoa kuhusu maeneo aliyotembelea.

Andrea Wulf, mtaalam wa historia ya Humboldt kamwe hakubaliani mtazamo huo. Anasema kwamba Humboldt alipingana na dhana za ukoloni na utumwa na aliunga mkono mapinduzi ya Venezuela: "Aliongelea kuhusu ‘ushenzi wa wastaarabu’ alipoona vitendo vya wakoloni na wamisionari dhidi ya wenyeji wa asili.” Wulf anaongezea kuwa Humboldt pia alikosoa mgawanyo wa ardhi usio wa haki, kulazimishwa kilimo cha zao moja, vitendo vya ukatili na hali duni ya wafanyakazi kwenye makoloni.

Mwanahistoria wa Munich, Frank Holl naye anapinga kwa nguvu tuhuma za vuguvugu la Berlin akieleza kuwa maandiko ya mtu huyu maarufu ni uthibitisho wa kile alichokiamini. Kulingana na Holl, Humboldt alitanabaisha kuwa pasingekuwa na furaha ya kudumu Bara Amerika hadi pale, “jamii duni zitakaponufaika na faida zitokanazo na maendeleo yanayoletwa na ustaarabu pamoja na mpangilio bora wa kijamii lakini bila ya kudharauliwa utu wao kutokana na ukandamizaji mrefu ". Holl anatetea hoja yake kwa kusema, huu “ni mtazamo ulio wazi kabisa wa kupinga ukoloni na kutetea jamhuri” uliotolewa kwa namna ambayo “kwa namna yoyote siyo kwa woga au kwa fumbo ".

Licha ya sifa hizi kutoka kwa washabiki wake, sanamu ya mwanasayansi huyu mashuhuri imeonekana kuwa nyufa chache wakati wa matukio ya kumbukumbu ya miaka 250 ya kuzaliwa kwake. Hata hivyo kuonekana kwa nyufa hizo hakujabadili umuhimu wa Alexander von Humboldt kwenye tafiti za mambo ya asili na matokeo ya tafiti hizo.