Mfumo wa Shule

Tisch mit Buntstiften © Goethe-Institut/ Gina Bolle

Nchini Ujerumani, kuna elimu ya lazima: Watoto wanapaswa kuhudhuria shule kwa kipindi cha miaka 9. Mwaka wa shule huanza Agosti au Septemba na kuhudumu hadi Juni au Julai, kulingana na jimbo.

Elimu ya Lazima na Gharama

Wanafunzi mara nyingi huenda katika shule za serikali. Katika shule hizi, hakuna ada ya shule. Gharama ndogo huweza kujitokeza kwa ajili ya nakala, vifaa au ziara. Katika shule za kibinafsi, ni sharti kulipa ada ya shule.

Mtoto wako hafahamu Kijerumani vizuri? Anahitaji msaada maalum wa kujifunza Kijerumani? Basi wasiliana moja kwa moja na shule.

Aina za Shule

Kuna aina mbalimbali za shule. Watoto wote huanza katika shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka 6 au 7. Baada ya darasa la 4, watoto huenda katika shule ya ngazi inayofuata. Shule ya msingi hutoa pendekezo katika mwaka wa 4 wa shule kuhusu shule inayofaa kwa mtoto wako. Kuna aina tofauti za shule za ngazi za juu, kulingana na jimbo:

Hauptschule/Mittelschule (Darasa la 5 hadi la 9 au 10): Katika Hauptschule kuna masomo ya vitendo kama ufundi au michoro ya kiufundi. Hapa, mwanafunzi hupata cheti cha schule ya Hauptschule, yaani cheti cha Hauptschule cha sifa baada ya darasa la 9. Si kila jimbo lina Hauptschule. Mara nyingi pia kuna Mittelschule. Katika Mittelschule, wanafunzi huwa na uzoefu mwingi wa vitendo. Hapa wanaweza kupata cheti cha Mittelschule au cheti cha sifa cha Mittelschule baada ya darasa la 9. Pia, wanaweza kupata cheti cha kati cha shule baada ya darasa la 10. Baada ya hapo, wanaweza kujifunza taaluma au kuendelea na shule ya juu zaidi.

Realschule (Darasa la 5 hadi 10): Realschule ni shule ya juu zaidi. Hapa, mwanafunzi hupata cheti cha Realschulabschluss. Baada ya hapo, wanaweza kujifunza taaluma au kuendelea na shule nyingine ya juu.

Gymnasium (Darasa la 5 hadi 12/13): Katika Gymnasium, mwanafunzi hupata Abitur na anaweza kwenda kusoma katika chuo kikuu. Katika Gymnasium, mara nyingi mwanafunzi hujifunza lugha 2–3 za kigeni, kama vile Kiingereza na Kifaransa. Wanafunzi hupata Abitur baada ya darasa la 12 (G8) au baada ya darasa la 13 (G9), kulingana na jimbo.

Gesamtschule (Darasa la 5 hadi 13): Katika baadhi ya majimbo kuna Gesamtschule. Hapa, Hauptschule, Realschule na Gymnasium zimo katika jengo moja. Mwanafunzi anaweza kupata cheti cha Hauptschulabschluss, Realschulabschluss au Abitur. Kama mtoto angependa kubadilisha shule, kwa mfano kutoka Hauptschule kwenda Realschule, ni rahisi zaidi. Katika shule zilizotenganishwa, kubadilisha shule kunawezekana pia, lakini si rahisi sana.

Shule Maalum: Katika kila jimbo kuna shule za lugha mbili, shule za msaada wa kielimu, shule za kitaaluma na shule za juu za ufundi na kazi. Maelezo ya kina zaidi yanapatikana katika michoro yetu ya maelezo.

Muda wa Shule na Malezi ya Alasiri

Katika shule nyingi, masomo hutamatika mchana au mapema alasiri (saa 2 au 3 mchana). Baada ya hapo, mtoto anaweza kwenda kwenye huduma ya malezi ya alasiri, kwa mfano kituo cha watoto. Hapo mtoto hubaki hadi magharabi. Hupata chakula na msaada katika kazi ya ziada. Huduma za vituo vya watoto hulipiwa na mzazi.

Kuna shule za kutwa nzima zinazo ongezeka. Katika shule hizi, watoto hubaki mchana kutwa, mara nyingi hadi saa 10 au 11 machweo. Wanapata chamcha na msaada wa kazi za ziada. Mara nyingi watoto huweza kushiriki kozi maalum kama michezo, kuchora au maigizo. Shule za serikali za kutwa nzima hazina ada. Katika shule za kibinafsi za kutwa nzima, ni sharti kulipa ada ya shule.

Masomo ya Shuleni

Watoto hupata masomo mbalimbali shuleni. Kati ya hayo ni pamoja na somo la michezo. Mara nyingi pia kuna mafunzo ya kuogelea. Katika shule nyingi kuna somo la dini ya Kikristo. Hata hivyo, unaweza kujiengua kutoka somo la dini na si lazima kuhudhuria. Badala yake, kuna somo la maadili au, katika baadhi ya shule,kuna masomo ya dini nyingine (kwa mfano Uislamu au Uyahudi).

Ikiwa mtoto wako ana changamoto katika somo fulani, anaweza kupata msaada wa ziada. Hii inaweza kuwa kutoka kwa mkufunzi binafsi au shule ya mafunzo ya ziada. Mafunzo binafsi huwa ya gharama ya nafuu zaidi.

Shughuli Nje ya Masomo

Watoto wa shule mara nyingi hufanya ziara ya darasa, mara moja kwa mwaka. Hii hudumu kwa siku 3 hadi 5. Darasa huenda pamoja katika mji au eneo jingine. Pia kuna siku za matembezi ambapo watoto huenda kwa matembezi ya pamoja. Kwa njia hii, watoto hujifunza kuhusu historia, tamaduni na mazingira. Shule pia hufanya sherehe za shule ambapo huweza kuwa na maigizo au tamasha kutoka kwa wanafunzi.

Wazazi

Kila shule ina wawakilishi wa wazazi: Hawa ni wazazi wanaoshirikiana na shule. Mara kadhaa kwa mwaka, kuna mikutano ya wazazi. Wazazi hupokea taarifa muhimu kutoka kwa wakufunzi na huweza kufahamiana. Unaweza pia kupanga miadi na mkufunzi kuzungumza naye peke yako. Hii huitwa Elterngespräch (mazungumzo na mzazi). Wazazi hujulishwa: Mtoto anafanyaje shuleni? Utendaji wake ukoje? Kuna changamoto yoyote?

Maswali ya Mara kwa Mara

Tufuatilie