Mafunzo ya Ufundi

Werkbank mit Holz, wo zwei Personen ein Holz vermessen © Goethe-Institut

Katika mafunzo ya ufundi stadi mtu hujifunza taaluma fulani. Kuna mafunzo mengi ya aina tofauti, kama vile mfanyakazi wa kutengeneza mikate, mtaalamu wa umeme, muuguzi, mchungaji bustani au mlezi wa watoto.

Viza, Cheti cha Kumaliza Mafunzo na Stashahada

Ungependa kufanya mafunzo ya ufundi stadi nchini Ujerumani? Na hauji kutoka Umoja wa Ulaya (EU) au kutoka Eneo la Kiuchumi la Ulaya (EWR)? Basi unahitaji viza.. Viza hupatikana katika Ubalozi wa Ujerumani (au Ubalozi Mdogo wa Ujerumani) katika nchi yako.

Umehitimu mafunzo ya ufundi stadi? Makampuni mengi yanatafuta wataalamu waliohitimu. Unaweza kuomba kazi. Mara nyingi unahitaji cheti kwa ajili ya nafasi ya kazi. Cheti ni hati rasmi yenye taarifa kuhusu mafunzo yako au taaluma yako. Una vyeti kutoka nchi yako? Vipeleke vitafsiriwe na vidhibitishwe. Mara nyingi unahitaji pia kukaguliwa vyeti hivyo. Hii itakuwezesha kupata kazi kwa urahisi zaidi. Maelezo zaidi unaweza kuyapata katika sehemu ya Kutafuta Ajira.

Kutafuta Mafunzo ya Ufundi Stadi

Mafunzo ya ufundi stadi yanaweza kufanyika katika makampuni mengi na katika karibia sekta zote. Kwa mafunzo hayo unahitaji angalau kuwa na cheti cha shule ya upili. Wakati mwingine unahitaji cheti cha shule ya kati au hata kidato cha sita (rejea: sehemu ya Mfumo wa Elimu). Bila cheti cha shule itakuwa vigumu sana kupata nafasi ya mafunzo. Nafasi za mafunzo hupatikana kama vile nafasi za kazi. Unahitaji pia kuandika maombi. Katika sehemu ya Kutafuta Kazi utapata maelezo na ushauri zaidi kuhusu maombi na utafutaji kazi.

Kila mji kuna Kituo cha Taarifa za Kitaaluma (BIZ). Wafanyakazi wa kituo hicho watakushauri na kukuauni kutafuta nafasi ya mafunzo. Kituo hiki kinapatikana kupitia Idara ya Ajira katika mji wako.

Mchakato wa Mafunzo ya Ufundi Stadi

Kuna aina 2 za mafunzo ya ufundi stadi: mafunzo ya shule na mafunzo ya mchanganyiko. Mafunzo ya shule hufanyika tu katika shule za ufundi maalum. Kwa hivyo unahitaji cheti cha shule na wakati mwingine uzoefu zaidi, kama vile mafunzo ya vitendo.

Mafunzo mchanganyiko yanajulikana pia kama mafunzo ya kiwandani. Nchini Ujerumani, mafunzo ya mchanganyiko ndiyo yanayopatikana zaidi. Hapa kuna sehemu ya vitendo na sehemu ya nadharia. Mafunzo ya vitendo hufanyika moja kwa moja katika kampuni. Pia huenda katika shule ya ufundi kujifunza nadharia ya taaluma hiyo. Pia kuna masomo ya jumla kama lugha ya Kijerumani, siasa au michezo.

Kazini unafanya mafunzo ya vitendo. Hufanya kazi siku 3 hadi 4 kwa juma na huenda shuleni kwa masaa 8 hadi 12 kwa juma. Au unakuwa majuma machache kazini na majuma machache shuleni.

Baada ya nusu ya mafunzo, unahitajika kufanya mtihani wa kati. Wanagenzi wa mafunzo (Azubis) huonyesha walichojifunza. Mwisho wa mafunzo kuna mtihani wa mwisho. Baada ya hapo wagenzi hupata cheti cha mafunzo. Cheti hiki ni Cha natija iwapo ungependa kupata kazi. Maelezo zaidi yapo katika sehemu ya Kutafuta Ajira.

Muda wa Mafunzo ya Ufundi Stadi

Mafunzo ya ufundi stadi kawaida hudumu kati ya miaka 2 hadi 3.5. Hii inategemea taaluma na cheti cha shule. Kwa waliohitimu kidato cha sita, mafunzo huwa mafupi zaidi. Katika mafunzo unapata likizo ya angalau siku 24 au majuma 4 kwa mwaka. Hii inapatikana tu wakati shule ya ufundi ina likizo na imefungwa.

Kuna mafunzo ya taaluma yanayoweza kufanyika kwa muda mfupi kama vile;katika huduma za watoto, uuguzi wa wazee, huduma za chakula au urembo. Mara nyingi haya ni mafunzo ya shule ya ufundi. Mafunzo ya shule ya ufundi hudumu kati ya mwaka 1 hadi 3.5. Utapata maelezo zaidi kutoka kwa Idara ya Ajira katika mji wako.

Mshahara

Unapofanya mafunzo ya mchanganyiko nchini Ujerumani, utalipwa mshahara mdogo. Mwajiri wako atakulipa mshahara. Kiasi cha mshahara hutofautiana kulingana na taaluma na eneo unalofanyia kazi. Kawaida mshahara huongezeka baada ya kila mwaka wa mafunzo. Wakati mwingi mshahara haukidhi gharama zote kama; kodi ya nyumba, chakula, burudani n.k. Kuna msaada wa kifedha, kwa mfano BAföG au Msaada wa Mafunzo ya Ufundi (BAB). Uliza Idara ya Ajira katika mji wako kuhusu hili.

Kwenye mafunzo ya shule ya ufundi hupokei mshahara. Wakati mwingine unahitaji hata kulipia ada ya shule.

Maswali ya Mara kwa Mara

Tufuatilie