Simu ya Rununu na Mtandao

Ungependa kupiga simu, kutumia mtandao, kusoga na kutuma ujumbe mfupi? Utahitaji kupata mtoa huduma wa simu. Nchini Ujerumani kuna watoa huduma wengi wa simu za rununu. Unaweza kuchagua kati ya mikataba au laini za malipo ya kabla, zenye gharama tofauti. Unapiga simu mara nyingi? Ungependa kutumia mtandao ukiwa safarini? Chagua mpango unaokufaa.

Audio-Player: Artikel anhören

Artikel anhören

Handy und Internet

Person bedient ein Smartphone © Goethe-Institut/ Gina Bolle

Watoa Huduma wa Simu na Bei

Kuna baadhi ya mipango inayokuwezesha kupiga simu na kutuma ujumbe bila kikomo. Pia kuna mipango yenye kiasi maalum cha kifurushi cha data . Data hii hutumika kuperuzi mitandaoni ukiwa nje. Ukimaliza data yako, unaweza kununua nyingine. Jihadhari: hii huongeza gharama. Wakati mwingine data huongezwa bila ya mwongozo wa mkono. Sitisha huduma hiyo ili kuepuka kulipa zaidi. Nunua data ya ziada tu kama kweli unahitaji. Kuna pia mipango yenye kikomo au kifurushi maalum. Hapa utalipia kila simu, kila ujumbe mfupi na kila utumiaji wa mtandao tu unapozitumia huduma hizo.

Linganisha punguzo mbalimbali. Unaweza kufanya hivyo kwenye tovuti za kulinganisha:
 

Simu za Kimataifa

Ungependa kupiga simu kutoka Ujerumani kwenda nje ya nchi? Kupitia simu ya mezani au simu ya rununu, inaweza kuwa ghali sana. Tumia WhatsApp, Skype au huduma nyingine kama hizo. Kwa njia hiyo unatumia mtandao na huna gharama za ziada. Pia unaweza kutumia kadi za simu au vocha kupiga nje ya nchi. Hii ni nafuu zaidi. Unaweza kupata kadi hizi katika maduka makubwa au maduka mengine.

Unasafiri mara kwa mara na ungependa kutumia laini yako ya Kijerumani ukiwa nje? Ndani ya EU, Norwe, Isilandi na Liechtenstein unaweza kupiga simu bila gharama za ziada. Katika nchi nyingine, inaweza kuwa ghali. Angalia ada za huduma za kimataifa kwa ujumbe mfupi, simu na mtandao. Pata taarifa mapema kuhusu gharama. Unaweza kuzima data za huduma za kimataifa ukiwa nje na kutumia mtandao kupitia mitandao ya bila nyaya (WLAN) kama kwenye hoteli au mikahawa.

Kuna pia ada maalum za mawasiliano ya kimataifa. Pata maelezo zaidi kutoka kwa watoa huduma wa simu za rununu.

Mkataba wa Simu ya Rununu

Unaweza kuingia mkataba na mtoa huduma wa simu ya rununu. Ni vyema kwenda dukani na kupata ushauri. Tahadhari: Usitie sahihi kwenye mkataba ambao hujauelewa. Soma mkataba kwa makini sana. Tafuta msaada wa kutafsiri. Unaweza pia kuingia mkataba kupitia tovuti, kuutia sahihi na kuutuma kwa mtoa huduma. Mtoa huduma atahitaji kuona kitambulisho chako au pasi yako ya kusafiria pamoja na cheti cha kujisajili mahali unapoishi.

Mikataba ya simu mara nyingi hudumu kwa mwaka mmoja hadi miwili. Kuivunja kabla ya muda si rahisi. Malipo ya bili hufanyika mwishoni mwa mwezi. Baada ya muda wa chini wa mkataba kutamatika, unaweza kuuvunja kwa kutoa ilani ya mwezi mmoja.

Laini ya kulipiwa kabla ya matumizi

Njia nyingine ni kutumia laini ya kulipiwa kabla ya matumizi. Unaweza kununua laini hizi kwa bei nafuu kwenye maduka makubwa, vituo vya mafuta au kwenye vibanda.

Ulinunua laini ya kulipiwa kabla ya matumizi, moja kwa moja kutoka kwa mtoa huduma? Basi unaweza kuiwasha dukani. Utahitaji kitambulisho au pasi. Wakati mwingine pia utahitaji kibali cha ukaazi. Utauniwa katika mchakato huo. Uliponunua laini hiyo, kwa mfano katika duka kubwa? Basi unaweza kuthibitisha utambulisho wako kupitia video au katika tawi la posta ya Ujerumani.

Kisha utahitaji kuweka salio. Salio unaweza kununua dukani au kwenye vibanda. Kwenye vocha za salio kuna namba ndefu. Sharti uingize namba hiyo kwenye simu. Wakati mwingine unaweza pia kununua salio moja kwa moja kupitia mpango wa mtoa huduma. Salio litakatwa unapopiga simu, kutuma ujumbe mfupi au kutumia mtandao.

WiFi

Ungependa kutumia mtandao bure? Katika mikahawa, maktaba au majengo ya umma mara nyingi kuna mtandao wa bila nyaya ya bure. Mtandaoni kuna tovuti zinazokuonyesha mitandao ya bila nyaya iliyo karibu nawe. Tahadhari: WiFi nyingi hazina usalama. Watu wengine usiowatarajia wanaweza pia kuona taarifa zako binafsi za siri.

Mtandao Nyumbani

Kuna njia na bei tofauti za kuunganisha mtandao chengoni. Hapa pia unapaswa kujiuliza: Unahitaji nini? Ungependa tu mtandao au pia simu ya mezani? Unatumia mtandao mara nyingi lakini mara chache kutazama filamu au kusikiliza muziki? Basi si lazima kuwa na kasi ya juu sana ya mtandao. Unatumia vifaa vingi kwa wakati mmoja, unafanya kazi kwa kipakatalishi ukiwa chengoni, unatazama filamu nyingi kwa ubora wa juu au unafanya simu nyingi za video na akraba? Basi huenda utahitaji muunganisho wa kasi zaidi.

Angalia ofa mbalimbali kwenye tovuti za kulinganisha: Utaingia mkataba na mtoa huduma wa mtandao. Hakuna chaguo la malipo ya kabla hapa. Soma mkataba kwa makini. Tia sahihi tu kama umeelewa kila kitu. Tahadhari: Mara nyingine ada ya kila mwezi huwa nafuu mwanzoni, lakini baada ya miezi kadhaa inakuwa ghali zaidi. Mikataba mara nyingi hudumu kwa miezi 12 hadi 24. Muda wa ilani mara nyingi ni sawa na ya mikataba ya simu. Kuna pia bei zisizo na muda maalum wa mkataba.

Maswali ya Mara kwa Mara

Tufuatilie