Siasa na Jamii

Menschenmenge mit Regenbogenflagge © Goethe-Institut/ Gina Bolle

Ujerumani ni nchi ya kidemokrasia. Wananchi wana haki ya kuwatueua watawala wao pamoja na sheria zitakazotungwa. Raia huteua serikali yao. Kila mja anaweza kushiriki katika maisha ya kisiasa kwa mfano kupitia asasi, au taasisi nyingine za kiraia, mashirika ya wafanyakazi na vyama vya siasa.

Audio-Player: Artikel anhören

Artikel anhören

Politik und Gesellschaft

Katiba

Katiba ya Ujerumani huitwa Grundgesetz. Ndani ya Grundgesetz mna sheria za msingi zinazotawala aushi ya pamoja nchini Ujerumani.

Ujerumani pia ni dola linaloongozwa na utawala wa sheria. Waja wote ni sawa mbele ya sheria—bila kujali umri, jinsia, asili, au dini. Mja yeyote anayehisi ametendewa jambo lisilo la haki anaweza kufungua mashtaka kule mahakamani.

Ujerumani ni taifa la kijamii. Serikali ina jukumu la kuhakikisha ustawi wa waja wake. Kuna huduma za lazima kama bima ya afya, ruzuku ya wastaafu, na msaada wa kijamii—ikiwemo posho kwa wasio na ajira. Kila mja ana haki ya maisha yenye taadhima.

Ujerumani ni muungano wa majimbo. Kuna majimbo 16: Baden-Württemberg, Bayern, Berlin, Brandenburg, Bremen, Hamburg, Hessen, Mecklenburg-Vorpommern, Niedersachsen, Nordrhein-Westfalen, Rheinland-Pfalz, Saarland, Sachsen, Sachsen-Anhalt, Schleswig-Holstein, na Thüringen. Kila jimbo lina sheria zake, lakini pia kuna sheria zinazotumika nchi nzima.

Haki na Wajibu

Katika Grundgesetz kuna haki na wajibu wa waja wanaoishi Ujerumani. Baadhi ya haki hizi ni za kila mja — hizi ni haki za binadamu. Haki nyingine zinahusu raia wa Ujerumani pekee — hizi ni haki za raia.

Wajibu muhimu ni pamoja na:Wajibu wa kuhudhuria shule: Watoto na vijana wanapaswa kwenda shule. Wajibu wa kulipa kodi: Waja wote wanaopata kipato sharti walipe kodi. Wajibu wa kutii kanuni: Kila mja sharti azingatie kanuni.

Hizi ndizo haki kuu:
  • Heshima ya utu wa binadamu: Kila mja anapaswa kuheshimiwa.
  • Usawa: Waja wote wana haki sawa. Mfano, wanawake na wanaume wana haki sawa.
  • Usawa mbele ya sheria: Kila mja ni sawa mbele ya sheria.
  • Haki ya kutoa maoni: Waja wanaweza kuwasilisha mawazo yao.
  • Uhuru wa kukusanyika: Waja wanaweza kukongamana.
  • Uhuru wa kuhamia: Waja wanaweza kuishi na kukaa wanakotaka.
  • Uhuru wa kuchagua kazi: Waja wanaweza kuchagua kazi wanayoitaka.
Haki nyingine ni pamoja na ulinzi wa ndoa na akraba, uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kushiriki uchaguzi, na uhuru wa dini.

Utofauti na Uvumilivu

Ujerumani, kila mja ana uhuru wa kuchagua na kuabudu dini yake. Takribani theluthi moja ya waja hawana dini rasmi. Wengi wa Wajerumani ni Wakristo, aidha Wakatoliki au Waprotestanti. Sikukuu nyingi za Kikristo kama Krismasi na Pasaka ni sikukuu rasmi; waja wengi hawahudhurii kazi siku hizo. Kuna pia waja wengi wa dini nyingine wanaoishi Ujerumani.

Mashuleni, kuna somo la dini ya Kiprotestanti na Kikatoliki. Katika baadhi ya shule, pia kuna somo la dini ya Kiorthodoksi, ya Kiyahudi na ya Kiislamu. Wazazi huamua kama mtoto wao atahudhuria somo la dini, na la dini gani.

Waja nchini Ujerumani wanaweza kuishi kwa uwazi kulingana na mwelekeo wao wa kingono. Hii ina maana kuwa mahusiano ya jinsia moja, mahusiano ya waja wa jinsia mbili, waja waliobadili jinsia na waja wa jinsia mbili mseto ni sehemu ya aushi ya kila siku, sawa na mahusiano ya kawaida kati ya wanaume na wanawake. Harakati za LGBTQ zina nafasi muhimu. LGBTQ ni jumuiya ya wasagaji, mashoga, wanaopenda jinsia zote mbili, waliobadili jinsia, na watu wa jinsia tofauti. Wanalindwa kisheria. Alama yao ni bendera ya upinde wa mvua.

Tangu 1 Oktoba 2017, wanandoa wa jinsia moja — mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke — wanaweza kufunga ndoa nchini Ujerumani. Wana haki sawa na majukumu sawa. Mfano: wanaweza kuasili watoto, kuchukua jina la mwenza wao na kuwajibika kwa kila mmoja.

Iwapo haki hizi hazitaheshimiwa, kunaweza kuwa na suala la ubaguzi. Tafadhali soma pia maandiko yetu "Kushughulikia Ubaguzi".

Vyama na Uchaguzi

Katika demokrasia kuna uchaguzi, ndivyo ilivyo Ujerumani. Uchaguzi sharti uwe wa siri, wa wote na huru. Wananchi huamua nani atawatawala.

Vyama vya siasa nchini Ujerumani vina mipango na malengo mbalimbali. Vyama vikubwa ni: SPD (Chama cha Kisoshalisti cha Kidemokrasia cha Ujerumani)
CDU (Chama cha Kidemokrasia cha Kikristo)
Bündnis 90/Die Grünen (Muungano wa 90/Chama cha Kijani)
FDP (Chama cha Demokrasia Huria)
AfD (Mbadala kwa Ujerumani)
Die Linke (Chama cha Kushoto)
Pia, kuna vyama vingine vingi vidogo. Maelezo zaidi kuhusu vyama hivi na mipango yao inapatikana kwenye tovuti ya Kituo cha Shirikisho cha Elimu ya Siasa: Vyama vya Siasa nchini Ujerumani.

Nani anaruhusiwa kushiriki uchaguzi? Haki ya kushiriki uchaguzi hutofautiana kulingana na aina ya uchaguzi:
Uchaguzi wa Bunge la Shirikisho na chaguzi za majimbo: Raia wa Ujerumani wenye umri wa miaka 18 au zaidi wanaweza kushiriki uchaguzi. Katika baadhi ya majimbo (kama vile Baden-Württemberg, Brandenburg, Bremen, Hamburg na Schleswig-Holstein), vijana wa miaka 16 wanaweza kushiriki uchaguzi katika uchaguzi wa majimbo, lakini hawawezi kugombea. Kugombea kunaruhusiwa kuanzia miaka 18.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa Raia wa Umoja wa Ulaya wanaoishi Ujerumani kwa zaidi ya miezi mitatu wanaweza kushiriki uchaguzi.
Katika majimbo ya Bayern, Hessen, Rheinland-Pfalz, Saarland na Sachsen, wapiga kura sharti wawe na umri wa miaka 18. Katika majimbo mengine, unaweza kushiriki kura ukiwa na miaka 16.Uchaguzi wa Bunge la Ulaya: Raia wote wa EU wenye umri wa miaka 18 au zaidi wanaweza kushiriki kura.

Unatoka nchi isiyokuwa ya Umoja wa Ulaya? Kwa bahati mbaya, huwezi kupiga kura nchini Ujerumani. Lakini bado unaweza kushiriki katika maisha ya kijamii na ya kisiasa. Katika maeneo mengi, kuna mabaraza ya ushirikishwaji wa wahamiaji. Wahamiaji huchagua wajumbe wa mabaraza haya. Mabaraza haya yanawakilisha maslahi ya wahamiaji kisiasa na huauni kwa ushauri na msaada. Lengo ni kuboresha maisha ya pamoja kati ya wahamiaji na Wajerumani.

Maswali ya Mara kwa Mara

Tufuatilie