Afya

Schild vor einem Krankenhaus © Goethe-Institut/ Gina Bolle

Unajihisi muele kidogo tu? Kwa mfano una mafua au maumivu ya kichwa? Kwa ndwele ndogo ndogo, unaweza kununua dawa katika duka la dawa. Katika Ujerumani kuna maduka mengi ya dawa. Wataalamu wa dawa wanaweza kukuauni. Wanaweza kujibu maswali yako na kukuauni kupata dawa sahihi.

Audio-Player: Artikel anhören

Artikel anhören

Gesundheit

Duka la Dawa

Kwa ndwele nyingi, hautapata dawa bila ya kuwa na cheti cha daktari. Katika karatasi hiyo inaelezwa ni dawa gani unahitaji. Lazima daktari aandike cheti hicho. Ukiwa nacho, unaenda nacho dukani na unalipia tu sehemu ya gharama. Bima ya afya hulipa sehemu iliyobaki.

Maduka ya dawa kwa kawaida hufunguliwa Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa mbili macheo hadi saa kumi na mbili machweo, na Jumamosi hadi saa saba mchana. Katika miji mikubwa, baadhi ya maduka ya dawa hufunguliwa hadi saa mbili usiku. Kuna pia huduma ya dharura kwa siku ya Jumamosi, Jumapili na usiku.

Bima ya Afya

Bima ya afya ni lazima kwa waja wote wanaoishi Ujerumani. Tafadhali soma maelezo zaidi katika taarifa yetu ya “Bima.”

Ziara kwa Daktari

Unajihisi muele au unahitaji msaada wa matibabu? Ni bora kupanga miadi na daktari wa tiba ya jumla. Huyu ndiye anayejibu maswali ya awali kuhusu matatizo ya ndwele zako zote. Anaitwa pia daktari wa akraba. Ni natija kwenda kumuona daktari. Anaweza kukuauni na ukapona. Kama hawezi kukuauni, atakuelekeza kwa daktari bingwa.

Mtoto wako ni mgonjwa? Basi nenda kwa daktari wa watoto. Kwa kawaida unaweza kwenda kwa daktari kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Kwa Jumamosi, Jumapili na usiku, kuna huduma ya dharura ya kitabibu.

Kwa ajili ya kupata miadi, unaweza kupiga simu kwenye kliniki. Au unaweza kupanga miadi mtandaoni. Hii inawezekana kwa madaktari wengi. Ni rahisi na inafaa. Unaingia kwenye tovuti ya kliniki na kuchagua miadi. Unapokea uthibitisho unaoonyesha siku na saa ya kwenda kwa daktari. Mara nyingi kabla ya siku ya miadi unapokea ukumbusho kwa barua pepe au ujumbe mfupi (SMS) katika simu yako ya rununu.

Unapomtembelea daktari, unahitaji kadi kutoka kwa bima yako ya afya, inayoitwa kadi ya bima ya afya au kadi ya afya. Kwa mara ya kwanza, lazima ujaze fomu ya taarifa ya binafsi. Unaandika jina lako, anuani n.k. Wakati mwingine kliniki inahitaji inahitaji kufahamu magonjwa uliyonayo na kama umekuwa ukitumia dawa mara kwa mara.

Baada ya kujisajili, unasubiri katika chumba cha kusubiria. Utaitwa. Mara nyingi unasubiri dakika chache tu, lakini wakati mwingine unaweza kusubiri zaidi ya saa moja.

Katika chumba cha matibabu, daktari atauliza: Unasikia maumivu wapi? Tangu lini? Umewahi kuwa na maumivu haya kabla? Unapaswa kueleza matatizo yako kwa undani. Baada ya mazungumzo, utadadisiwa. Kisha utapewa majibu ya udadisi. Daktari atakuambia una ugonjwa gani na nini cha kufanya. Mara nyingi utapewa cheti cha dawa. Dawa hizo utazichukua katika duka la dawa. Wakati mwingine utapangiwa miadi kwa udadisi mwingine.

Hutalazimika kulipia ziada kwa daktari ikiwa una bima ya afya ya umma. Huduma za ziada binafsi sharti ulipie mwenyewe. Waja walio na bima ya afya ya binafsi hupokea bili. Wanailipia na baadae hulipwa na bima ya afya.

Taarifa ya Ugonjwa (Kujitaarifu kwa Ajira)

Wewe ni muele na hauwezi kufanya kazi? Lazima umwarifu mwajiri wako mara moja. Unamtaarifu mwajiri wako kuwa ni muele. Unapiga simu na kusema ni kwa muda gani ambao unatarajia kuwa mgonjwa.

Ulienda kwa daktari? Kama hauwezi kufanya kazi kutokana na uele, daktari atakuandikia kuwa wewe ni mgonjwa. Hii inaitwa pia cheti cha ugonjwa. Kinaeleza kuwa huwezi kufanya kazi na unatakiwa kubaki chengoni upumzike. Cheti hicho kinaonyesha muda wa mapumziko hayo. Hautapewa karatasi. Daktari atatuma taarifa moja kwa moja kwa bima ya afya. Mwajiri wako anaweza kuona taarifa hiyo mtandaoni.

Waajiri wengine watahitaji cheti cha ugonjwa kuanzia siku ya kwanza ya ugonjwa. Wengine kuanzia siku ya tatu. Unaweza kupiga simu kliniki ya daktari na kuomba cheti cha ugonjwa kwa uele mdogo kwa muda wa siku tano. Kama utaendelea kuwa muele kwa muda mrefu, sharti uende kwa daktari.

Madaktari Bingwa

Kuna aina nyingi za madaktari. Wana taaluma tofauti. Kwa hiyo wanaitwa madaktari bingwa. Hao ni wataalamu. Kwa mfano, kuna madaktari wa mifupa. Wanasimamia masuala ya mifupa na viungo. Kwa mfano, ukivunjika mkono. Madaktari wa wanawake hufanya ukaguzi wa kiafya kwa wanawake na kuwahudumia wajawazito. Kuna pia madaktari wa pua, koo na masikio na wengine wengi.

Mara nyingi daktari wa akraba atakuelekeza kwa daktari bingwa. Utapewa barua ya utambulisho. Baadaye, daktari wa akraba atafahamishwa kuhusu uele wako.

Wafahamu unahitaji daktari yupi bingwa? Basi unaweza kwenda moja kwa moja kwake. Si sharti wewe kuwa na barua ya utambulisho. Kwa daktari wa meno pia hauhitaji barua ya utambulisho.

Afya ya Ubongo

Unajihisi vibaya? Unahisi kuchoka na kuwa mnyonge? Siha ya mwili ni ya natija sana. Lakini sio mwili pekee unaoweza kuwa mgonjwa, bali pia ubongo. Hii inahusiana na mawazo na hisia. Changamoto, misukosuko, msongo wa mawazo, hofu au ukatili vinaweza kutufanya tuwe wagonjwa. Jali afya yako ya ubongo. Jitunze vizuri. Tafuta auni unapojisikia una huzuni, msongo wa mawazo au hofu.

Uchunguzi wa Kuzuia Magonjwa

Kwa kutumia udadisi wa kinga, magonjwa makubwa yanaweza kugunduliwa mapema na kutibiwa kwa haraka zaidi. Baadhi ya uchunguzi hulipiwa na bima ya afya. Udadisi mwingine unapaswa kuulipia mwenyewe.

Hata kwa watoto, kuna uchunguzi wa kinga. Ni natija sana. Kuna chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukizana kama surua, kikohozi kikuu na mafua mabaya. Tafadhali soma taarifa zetu kwenye maandishi “Kuishi na Watoto.”

Kuanzia umri wa miaka 35 kuna uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya figo, moyo na mishipa, kisukari na saratani. Kwa wanawake, kuna uchunguzi wa matiti kwa njia ya kupapasa. Wajawazito hupata uchunguzi wa kinga mara kwa mara.

Kulingana na jinsia, umri au historia ya magonjwa katika akraba, kuna udadisi maalum. Hata kwa waja wazima, chanjo ni muhimu. Zungumza na daktari wako.

Nambari Muhimu kwa Dharura

Waja wote walioko Ujerumani wanapaswa kufahamu nambari ya dharura ya polisi 110 na ya zima moto au huduma ya dharura ya afya 112. Kuna pia namba nyingine za msaada na ushauri. Soma maelezo zaidi katika maandishi yetu “Nifanye nini katika hali ya dharura?

Maswali Ya Mara kwa Mara

Tufuatilie