Kazi na Malengo

Kama taasisi ya utamaduni ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani inayofanya kazi duniani kote, tunafanya uchechemuzi wa maelewano baina ya Ujerumani, Ulaya na dunia kwa ujumla. Makubaliano ya awali kati yetu na Ofisi ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani ni msingi wa kazi hii. Kote duniani, tunatoa taarifa kuhusu hali anuwai ya kiutamaduni na kijamii ya Ujerumani na Ulaya. Vituo 158 vya Goethe-Institut katika nchi 98 pamoja na taasisi nyingi washirika vinaunda msingi thabiti wa mtandao wetu duniani. Ofisi ya Mambo ya Nje inaunga mkono kazi yetu kitaasisi. Kama shirika la hisani lililosajiliwa tunafanya kazi bila ya kuingiliwa katika msingi wa uhuru kisheria na hatufungamani na chama chochote cha siasa. Tunatengeneza takribani theluthi moja ya mapato yetu sisi wenyewe kupitia ada kwa ajili ya kozi za lugha na mitihani. Pia tunafadhiliwa na Umoja wa  Ulaya, wizara nyingine za serikali ya Ujerumani halikadhalika mashirika na makampuni ya ndani na nje ya Ujerumani.

Tunachangia kuamirisha lugha ya Kijerumani katika mifumo ya elimu ya nchi wenyeji. Tunasaidia zaidi ya shule 100,000 duniani kote katika kutoa mafundisho bora ya KIjerumani, na kutoa msukumo wa mafunzo ya juu ya kitaalamu na sifa za walimu wa Kijerumani. Zaidi ya hayo, tunatoa wigo wa kozi za lugha kuanzia kozi za kawaida za Kijerumani hadi kozi za weledi wa lugha na semina ili kukuza ufahamu wa kijamii na kitamaduni. Huduma zetu zinajumuisha kozi kwa njia ya intaneti na programu binafsi za ujifunzaji. Kila mwaka, watu zaidi ya nusu milioni hufanya mtihani wa Kijerumani katika kituo cha Goethe-Institut au miongoni mwa washirika wetu. Tukiwa na wigo mpana wa programu za elimu na taarifa, tunasaidia hasa wanafunzi na wafanyakazi wenye ujuzi kutoka nje katika safari zao za kuja Ujerumani. 

Tunaamini katika nguvu ya ufungamano wa kimataifa katika utamaduni. Matukio yetu ya kiutamaduni yapatayo 20,000 kwa mwaka hufanyika kwa ushirika na serikali na taasisi zisizo za kiserikali na harakati kutoka asasi za kiraia katika nchi wenyeji. Tunastahilisha, kushauri na kukutanisha wataalamu wa utamaduni na kusaidia katika ujenzi wa miundombinu endelevu ya uchumi wa kazi za kiutamaduni na kazi bunifu kupitia mafunzo ya juu kwa wajasiriamali wa sekta ya utamaduni au kuyapeleka makampuni ya kazi bunifu kimataifa. Kupitia programu zetu za makazi, mashirikiano na uzalishaji wa pamoja, tunachochea ujenzi wa mtandao wa wataalamu wa utamaduni duniani. Tunatoa nafasi na wigo salama wa kubadilishana fikra kwa wadau kutoka asasi za kiraia. Hatuachi mijadala ya kidemokrasia, hata katika nyakati ngumu. Katika kazi yetu tunafuata maadili ya jamii ya kidemokrasia na mabadiliko, inayoheshimu utawala wa sheria. 

Kupitia programu zetu za kidijitali za taarifa na elimu katika lugha zaidi ya 60 na mtandao wa maktaba 95, tunatoa nafasi ya kujifunza, kukutana na kushiriki. Tunatumia teknolia za kisasa, kuchangamkia fursa za kufanya mambo kidijitali, na papo hapo tukitafakari faida zake kwa watu na jamii. Kwa mitindo mbalimbali kama vile safari za mafunzo kwa ajili ya kuzidisha maarifa, mikutano maalumu baina ya wataalamu, programu za kuwakutanisha vijana na matamasha ya kimataifa tunawezesha mawasiliano, kimsingi, dunia nzima.

Goethe-Tanzania

Goethe-Institut nchini Tanzania

Goethe-Institut Tanzania ilianza mwaka 1962 na kufungwa kwa muda Machi 1998. Kufunguliwa tena kwa taasisi hii kulifanyika Septemba 3, 2008, na kushuhudiwa na Rais wa GI Prof. Dr. Klaus -Dieter Lehmann, Garden Avenue (Dar es Salaam). Wakati wa kutafuta ofisi ya kudumu, ofisi ya muda ilitumia majengo ya Kituo cha utamaduni cha Ufaransa, Alliance Française de Dar es Salaam.

Tangu Novemba 11, 2008, Goethe-Institut imekodi majengo ya ubalozi wa zamani wa Poland, Mtaa wa Upanga. Jengo hili jipya la taasisi lilifunguliwa rasmi na Guido Westerwelle, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani, Aprili 6, 2010.

Goethe-Institut Tanzania inaratibu na kusaidia kufanyika kwa wigo mpana wa shughuli za utamaduni zinazowasilisha utamaduni wa Ujerumani nchi za nje na shughuli za mwingiliano wa tamaduni tofauti.

Ofisi zetu za lugha hutoa kozi za lugha, warsha na semina kwa walimu katika fani ya lugha ya Kijerumani kama lugha ya kigeni na programu pana ya mitihani.