Saa zako za kazi zinategemea kazi yako na mkataba wa ajira (kwa maelezo zaidi soma maandishi kuhusu “
Kuanza Kazi”). Kwa mfano, kama wewe ni muuguzi katika hospitali, unafanya kazi kwa zamu: wakati mwingine macheo, wakati mwingine machweo au usiku.
Katika ofisi, mara nyingi kunakuwa na saa za kazi zilizopangwa vizuri. Unaanza kazi macheo na baada ya saa 8 au 9 unakamilisha kazi. Mara nyingine ofisini kuna mfumo wa muda unaobadilika (flexible), yaani unaweza kuanza kazi saa 8 au saa 9 macheo na ukakamilisha mapema au kwa kuchelewa. Katika kila kazi kuna angalau mapumziko, mojawapo mara nyingi ni ya chamcha ya dakika 30 hadi 60. Waajiri wengi siku hizi wanaruhusu kazi kufanywa kutoka chengoni. Kwa kawaida, watu hufanya kazi kwa saa 38 hadi 40 kwa juma. Pia kuna uwezekano wa kufanya kazi kwa muda nusu wa masaa yote, kwa mfano asilimia 50. Hii ni sawa na saa 20 kwa juma. Kama una watoto au una kazi nyingine ya kujitegemea pembeni, huu ni mpango mzuri. Nchini Ujeruman kuna mshahara wa chini uliowekwa: waajiri hawaruhusiwi kulipa chini ya euro 12.41 kwa saa (kama ilivyo mwaka 2024).
Kila mfanyakazi ana idadi fulani ya siku za likizo kwa mwaka. Sharti uombe likizo hiyo rasmi kutoka kwa mkubwa wako kazini na ni sharti mkubwa wako akubali. Unaweza kugawa likizo hizi katika kipindi chote cha mwaka. Mara nyingi unaweza kuchagua wakati ambapo utachukua likizo. Lakini wakati mwingine huwezi kuchukua likizo madamu kuna kazi nyingi sana. Wakati mwingine lazima uchukue likizo kwa kuwa kampuni nzima iko likizoni. Katika kipindi cha likizo, unaendelea kulipwa mshahara wako.
Ukipatwa na uele, lazima umjulishe mwajiri wako mara moja na ujisajili kuwa muele. Hii inaitwa taarifa ya ugonjwa. Mara nyingi, waajiri wanahitaji cheti cha daktari baada ya siku 3 (yaani siku ya 4) za uele (tazama maandishi ya “Afya”). Wengine hutaka cheti hicho mapema zaidi. Unaweza kwenda au kupiga simu kwa daktari: kwa kawaida, unaweza kujisajili kwa simu kuwa muele. Daktari wako atatuma taarifa ya ugonjwa kwa njia ya kidigitali kwa kampuni yako ya bima ya afya. Mwajiri wako ataweza kuona taarifa hiyo mtandaoni. Hii inahusu waja walio na bima ya afya ya kiserikali. Kama una bima ya afya ya kibinafsi, unahitaji cheti cha karatasi. Utatakiwa kukipeleka mwenyewe.